Lakini mimi ni mtoto tu! Kwanini nahitaji kupanga bajeti?
Ubongo huwa tunatafuta njia mpya za kusaidia vijana kama wewe kukua na kufanikiwa. Ili kujua wasichana wanafikiria nini kuhusu fedha, tulisafiri kwenda vijiji vilivyopo Nakuru (Kenya), Mwanza na Shinyanga (Tanzania). Wasichana tulioongea nao wana fedha za kununulia vitu vidogo vidogo ambazo hutumia kununulia pipi na chipsi kama watoto waliopo jijini.
Tuliwauliza watoto kama wewe jinsi wanavyoweka akiba, wanavyotafuta kipato na wanavyotumia fedha zao.
Wengi wenu mlidhani kwamba elimu ni muhimu na mlisema kwamba mnaweka akiba ya fedha ili kununua vitu vya shule au vitu vinavyohusiana na malengo yenu ya kielimu. Pia, mlituambia mnapotunza fedha zenu. Tukagundua kwamba wengi wenu mnatunza fedha kwenye benki.
Pia tulitaka kujua jinsi watazamaji wetu wanavyofanya maamuzi ya fedha za kutumia na za kuweka akiba. Kwahiyo tuliwauliza kama mnapanga bajeti. Asilimia 80 walisema kwamba wanapanga bajeti ya matumizi ya fedha zao.
Tulifurahi sana kusikia kuhusu matumizi yenu ya fedha na tunathamini taarifa zote tulizozipata. Hii inaonesha kwamba elimu ya fedha ni muhimu kwa KILA MTU: inatusaidia kutawala fedha zetu na kuweza kufikia malengo yetu ya baadaye. Tunategemea kusikia toka kwa watazamaji wetu ili kupata mawazo YENU zaidi, ili tuweze kutengeneza vipindi vya Ubongo Kids ambavyo vitawasaidia kujifunza na kufanikiwa.